Zika: Kenya huenda ikajiondoa kwenye Olimpiki

Image caption Kenya ndio bingwa mtetezi wa riadha duniani

Kenya huenda ikajiondoa kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyoratibiwa kufanyika Brazil endapo hakutakuwa na suluhu dhabiti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Zika.

Mwenyekiti wa kamati ya olimpiki ya Kenya bwana Kipchoge Keino amenukuliwa akisema kuwa taifa hilo bingwa wa dunia katika riadha huenda likajiondoa ilikuzuia kuhatarisha maisha ya wanariadha wake wasiambukizwe maradhi ya homa ya Zika ambayo imeenea nchini Brazil.

''Hatuwezi kuwapeleka wanariadha wetu Brazil iwapo mlipuko wa ugonjwa wa Zika hautadhibitiwa'' alisema Kipchoge Keino

Vilevile ugonjwa huo ulizua taharuki baada ya kupatikana kwenye manii mate na hata kwa jasho ya mtu aliyeambukizwa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Zika:Kenya huenda ikajiondoa kwenye Olimpiki

Hakuna dawa yeyote ya kutibu ugonjwa huu kwa sasa wala hakuna kinga ila kuzuia usiumwe na mbu.

Kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC, imesema kuwa inaendelea kushauriana na kamati andalizi ya Rio2016 kwa nia ya kutathmini tishio la kuenea kwa ugonjwa huo.

Brazil imesema kuwa maeneo yatakayotumika katika mashindano hayo ya Olimpiki yatakuwa yakichunguzwa kila siku hadi wakati wa mashindano hayo.

Kenya ndio bingwa mtetezi wa riadha duniani na iwapo itajiondoa kutoka kwenye mashindano hayo basi athari yake itakuwa wazikatika riadha.