Mchujo wa New Hampshire umeanza

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kura ya maoni kwa sasa inaonyesha kuwa bwenyenye Donald Trump anaongoza washindani wenzake, kukiwemo aliyeshinda katika jimbo la Iowa, Ted Cruz na Marco Rubio katika chama cha Republicans.

Wakaazi wa jimbo la New Hampshire nchini Marekani wameanza utaratibu wa kuwateua wawaniaji viti wa vyama vya Democratic na Republican.

Wagombeaji nao wanasubiri kwa hamu na ghamu matokeo ya kura hii ya mchujo kwani hilo ni jimbo la pili kufanya shughuli hizo baada ya Iowa juma lililopita.

Kura ya maoni kwa sasa inaonyesha kuwa bwenyenye Donald Trump anaongoza washindani wenzake, kukiwemo aliyeshinda katika jimbo la Iowa, Ted Cruz na Marco Rubio katika chama cha Republicans.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Seneta Bernies Sanders yuko mbele sana ya mpinzani wake mkuu, Hillary Clinton kulingana na kura ya maoni

Kura ya maoni ya wagombeaji wa chama cha Democrats zinaonyesha kuwa Seneta Bernies Sanders yuko mbele sana ya mpinzani wake mkuu, Hillary Clinton.

Sanders, ambaye ni Senator wa jimbo jirani la Vermont, anatarajia kushika kasi zaidi iwapo atashinda katika jimbo hili muhimu.

Katika jimbo la Iowa alishindwa na Bi Clinton mkewe rais wa zamani Bill.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Katika mji mdogo wa Dixville Notch wakazi tayari wamekwisha piga kura zao na wamemchagua seneta Bernie Sanders na John Kasich.

Katika mji mdogo wa Dixville Notch wakazi tayari wamekwisha piga kura zao na wamemchagua seneta Bernie Sanders na John Kasich.

Kulingana na sheria ya New Hampshire ,miji yenye wakaazi wasiozidi 100 wanaweza kuomba ruhusa ya kupiga kura pindi saa inapogonga usiku wa manane.

Bwana Sanders,ambaye anatokea jimbo jirani la Vermont ambaye amekiri kuwa "ni msosholisti ", anakamia kupata ushindi mkubwa New Hampshire iliafufua kasi katika kampeini yake hususan baada ya kushindwa na bi Hillary Clinton huko Iowa juma lililopita.