Rais Zuma abadilisha msimamo wake

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Rais Jacob Zuma

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amebadilisha msimamo wake wa hapo awali na kuiambia mahakama ya kikatiba kwamba ripoti ya mlinzi wa umma kuhusu ukarabati wa nyumba yake ilikuwa ya haki.

Mawakili wake wamekubali kwamba alifanya makosa aliposhindwa kutimiza mapendekezo ya ripoti hiyo ,lakini wakaongezea kwamba matendo hayo ya rais hayakwenda kinyume na sheria,kama inavyodaiwa na upinzani.

Kwa sasa Mahakama ya juu nchini Afrika Kusini inaendelea kusikiza kesi ya upinzani kwamba rais wa taifa hilo ni lazima alipe dola milioni 23, fedha za umma zilizotumiwa kukarabati nyumba yake.

Ripoti ya mwaka 2014 imesema kuwa Jacob Zuma alifaidika kinyume cha sheria katika ukarabati huo ambao umeshirikisha kidimbwi cha kuogelea.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Nyumba ya Nkandla ya rais Zuma iliokarabatiwa kwa kutumia fedha za Umma

Amekubali kulipa fedha hizo na sasa kesi hiyo inahusu iwapo alivunja sheria kwa kuipuza ripoti hiyo.

Wapinzani wakiongozwa na aliyekuwa mwandani wa rais Zuma ambaye sasa amebadilika na kuwa mpinzani mkuu Julius Malema wameandamana hadi katika mahakama hiyo.

Maandamano hayo yalikuwa yakipinga ufisadi na kutolewa kwa nyadhfa fulani serikalini kwa upendeleo fulani,msemaji wake wa Chama chake cha Economic Freedom Fighers alisema.

Chama cha upinzani cha Democratic Alliance pia kilipanga maandamano yake nje ya mahakama ya Johannesburg ambapo kuna maafisa wengi wa polisi.

Chama cha bw.Zuma ANC kimeyataja maandamano hayo kuwa ya kisiasa.