Ashtakiwa kwa kumrusha burukenge mgahawani

Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Picha ya kijana alimrusha mgahawani burukenge huyo

Mtu mmoja mjini Florida anakabiliwa na mashtaka ya unyanyasaji baada ya kumtupa burukenge katika mgahawa mmoja wa chakula.

Joshua James mwenye umri wa miaka 23,ametuhumiwa kwa kumtupa mnyama huyo aliye hai kupitia dirisha la mgahawa huo wa Wendy.

Mamaake amesema kuwa alikuwa akitaka kumtania rafikiye aliyekuwa akifanya kazi katika mgahawa huo.

Mnyama huyo alikamatwa na kurudishwa msituni.

Bwana James kutoka eneo la Jupiter mjini Florida alimpata burukenge huyo katika upande mmoja wa barabara na kumbeba katika lori lake,kulingana na ripoti ya tume ya kuwahifadhi wanyama mjini Florida.

Baadaye alienda katika mgahawa huo huko Royal Palm Beach,ambapo aliagiza kinywaji katika dirisha la mgahawa huo kabla ya kumrusha nyama huyo mwenye urefu wa futi tatu kupitia dirisha hilo.

Kisa hicho kilitokea mnamo mwezi Octoba lakini mshukiwa amekamatwa na anazuiliwa kwa sasa.

Pia anakabiliwa na mashtaka ya umiliki wa mnyama huyo pamoja na usafirishaji wake kinyume cha sheria.