Mandla Mandela taabani kwa kuukubali Uislamu

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Chifu Mandla Mandela taabani kwa kuukubali Uislamu

Hatua ya mjukuu wa kiongozi mwanzilishi wa Afrika Kusini Nelson Mandela , Mandla, 42, kuslimu na kuoa mke wa nne imevutia hisia kali kutoka kwa viongozi wa kabila lake la AbaThembu.

Wazee hao viongozi wenza wa kabila la Mvezo iliyokuwa ya marehemu ya Mandela ''hawaamini kuwa Chifu mzima wa kabila la Mvezo anaweza kuasi tamaduni zake na kuiga zile za mke wake ''

Mandla alifunga ndoa yake ya nne na bi Rabia Clarke katika msikiti mmoja mjini Cape Town Afrika Kusini mwishoni mwa juma.

Kongamano la viongozi wa jamii mbalimbali nchini Afrika Kusini ; The Congress of Traditional Leaders in South Africa (Contralesa) limeiambia BBC kuwa kuslimu kwa Chifu Mandla kutamzuia kutekeleza majukumu muhimu kuambatana na tamaduni za watu wa jamii ya Xhosa.

Chifu huyo wa kabila la Mvezo ambaye pia ni mbunge alitoa taarifa akiishukuru familia ya Rabia kwa kumruhusu afunge ndoa na mwana wao.

Haki miliki ya picha MandlaMandela
Image caption Chifu Mwelo Nonkonyane ameiambia BBC kuwa Mandela bila shaka atakabiliwa na changamoto tele.

''natoa shukrani kubwa kwa familia ya Rabia kwa kunikaribisha kwa dini ya kiislamu''

Shekh Ibrahim Gabriel aliyeendesha nikaa hiyo katika msikiti wa Kensington siku ya Jumamosi alithibitisha kuwa Mandla alislimu mwaka uliopita na kuwa ndoa hiyo iliendeshwa kwa misingi ya sharia ya kiislamu.

Chifu Mwelo Nonkonyane ameiambia BBC kuwa Mandela bila shaka atakabiliwa na changamoto tele.

''Sio mbaya eti kiongozi mmoja wetu ataamua kubadili dini yake ila tunachohoji ni uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake kama Chifu ipasavyo''

Viongozi wa kijamii hutakiwa mara kwa mara kutekeleza matambiko kwa sababu moja au nyengine.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption ''Chifu mzima wa kabila la Mvezo anawezaje kuasi tamaduni zake na kuiga zile za mke wake'' wanahoji wazee hao

Na hivyo Chifu Nonkonyane anashuku majukumu yatakinzana na dini hiyo mpya yake ya Uislamu.

'' Je ataweza kuwachinjia miungu wetu kafara ?''

Chifu Mandla sasa anamaswala mengi yanayohitaji ufumbuzi huku wengi wanaomuhudumia wakisema atahitajika kufanya maamuzi magumu hivi karibuni.

Kwanza anachokabiliwa nacho ni maelezo ya kwanini harusi yake haikuhudhuriwa na machifu wenzake wa kabila la Mvezo .

Wandani wanadokeza kuwa hawakukubaliana na uamuzi wake huo wala ndoa yake hiyo ambayo mkewe hakuonesha nia yeyote ya kutaka kuukumbatia wajibu wake kama mke wa kiongozi wa kabila la Aba thembu.

Video imeonekana katika mitandao ya kijamii inayomuonesha mrithi huyo wa kiti cha babu yake akiikariri ''Allah Akbar'' maanake ''Mungu ni mkubwa na hakuna aliye na uwezo zaidi yake''

Watumizi wengi wa mitandao ya kijamii walihoji iwapo tofauti yao wawili itaruhusu ndoa hiyo kusimama.