Historia ya Amama Mbabazi

Haki miliki ya picha
Image caption John Patrick Amama Mbabazi

Tangu atangaze nia ya kumpinga mwandani wake wa miaka mingi rais Yoweri Museveni, watu wengi walijiuliza kwani huyu Amama Mbambazi ni nani ?

Jina lake kamili ni John Patrick Amama Mbabazi, Waziri mkuu wa zamani wa Uganda.

Alizaliwa Januari 16, mwaka 1949 katika kijiji cha Mparo katika Wilaya ya Kabale.

Mbabazi alisomea shule ya upili ya Kigezi iliyoko Butobere na kisha akahitimu masomo ya juu katika shule ya upili ya Ntare .

Waziri huyu mkuu wa zamani alihitimu na shahada ya sheria kutoka chuo kikuu cha Makerere.

Mbabazi ni wakili wa mahakama za Uganda tangu mwaka 1977.

Aliwahi kuhudumu kama wakili wa umma katika afisi ya mwanasheria mkuu kati ya mwaka wa 1976 - 1978.

Mbabazi alihudumu kama waziri mkuu wa 10 wa Uganda kati ya mwaka wa 2011 hadi Septemba 2014.

Alikuwa kiungo muhimu cha utawala wa rais Museveni na walishirikiana kwa kipindi kirefu hususan wakiwa katika vuguvu la NRM lililopamabana dhidi ya tawala za kiimla nchini humo.

Image caption Wafuasi wa Mbabazi

Kati ya mwaka 1986 na 1992, alifanya kazi kama mkuu wa usalama wa ndani.

Pia alikuwa waziri wa nchi katika afisi ya rais, anayeshughulikia masuala ya siasa.

Alihudumu kama mwanasheria mkuu na waziri wa sheria kati ya mwaka wa 2004 - 2006

Alikuwa mwakilishi wa eneo la Kinkiizi Magharibi katika bunge la taifa tangu mwaka wa 1996.

Alihudumu kama waziri wa Ulinzi kati ya mwaka wa 2006- 2008.

Pia alisimamia usalama wa ndani kati ya mwaka wa 2009-2011.

Image caption Kulikuwa na shinikizo la kuwakutanisha Besigye na Mbabazi lakini halikufaulu

Uhusiano wake na rais Museveni ulidorora baadaye na mwezi wa Septemba 2014 Museveni alipomchagua Ruhakana Rugunda rafiki wa karibu Mbabazi kuchua nafasi yake.

Wakati huo hatua hiyo ilitazamwa kama njia ya kumuadhibu Mbabazi kwa sababu alikuwa amekusudia kumpinga rais Museveni ndani ya NRM.

Na baada ya kimya Mbabazi alitangaza rasmi nia yake ya kuwania urai kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa YouTube.

Kupitia kwa taarifa aliyoichapisha kwenye mtandao wa Youtube, bwana Mbabazi aliahidi

''kufufua na kuleta muamko mpya nchini Uganda.''

Wakati huo alitangaza kuwa hataondoka katika NRM bali atasalia mumo humo na kuchuana dhidi ya mwandani wake wa zamani.

Hilo halikutendeka.

Rais Museveni tayari alikuwa ameidhinishwa na kamati kuu ya chama hicho japo hakuwa amepokea ithibati rasmi.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mbambazi alionja makali ya utawala wa Museveni alipokamatwa sawa na Besigye

Licha kutawala Uganda tangu mwaka wa 1986 Museveni alipuzilia mbali wazo la kumtaka asiwanie muhula wake wa nne.

Na kama ilivyotarajiwa Museveni alitumia vyombo vya dola kumdhibiti yeye pamoja na viongozi wengine wa upinzani.

Amama Mbabazi alikamatwa na polisi akiwa mjini Jinja barabarani akielekea mkutano wake wa kwanza wa hadhara na wafuasi wake mjini Mbale mashariki mwa nchi.

Polisi nchini Uganda walitoa taarifa kusema kuwa Mbabazi hana ruhusa ya kufanya mikutano yoyote ya kisiasa japo alikuwa amewataarifu.

Siku hiyo hiyo,mwanasiasa mwingine wa upinzani Kizza Besigye alikamatwa na polisi akiwa nyumbani kwake.

Daktari Besigye , ambaye ni kanali mstaafu wa jeshi alikamatwa akiwa barabarani akienda kuhutubia mkutano wa kisiasa wa chama chake cha Forum For Democratic Change.

Ilimbidi waziri huyo mkuu wa zamani kuwania urais nje ya NRM.

Na hivyo alitangaza nia yake ya kuwa mgombe huru.

Mbabazi alitangaza hilo Julai 31 2015 akiwa nyumbani kwake Kololo katika siku ya mwisho iliyoruhusiwa kisheria kurejesha fomu za uwaniaji wadhfa huo.

Image caption Je John Patrick Amama Mbabazi atatimiza ndoto yake?

''kamwe sitatoka NRM''.

''Lakini sitaweza kugombea urais katika tikiti ya chama hicho cha NRM ilihali vipengee vingi tu vya vya chama vinakiuka katiba ya nchi''.

'' sitawania urais kwa tikiti ya NRM lakini wakati wa uchaguzi nitawania urais'

''kama mwanzilishi wa chama ,wakili na mwananchi Mzalendo,sitajiingiza katika maswala yanayokiuka sheria''

Je John Patrick Amama Mbabazi atatimiza ndoto yake?