Christie ajiondoa mbio za urais Marekani

Christie Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Christie aliombwa na viongozi wa Republican awanie 2012 akasema hakuwa tayari

Mwanasiasa wa chama cha Republican Chris Christie amejiondoa kutoka kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais Marekani baada ya kutofana uchaguzi wa mchujo New Hampshire.

Gavana huyo wa New Jersey alitumia pesa nyingi na kufanya kampeni kwa muda mrefu zaidi kushinda wagombea wengine lakini bado akamaliza wa sita.

Bw Christie amejiunga na Carly Fiorina, afisa mkuu wa mtendaji wa kampuni ya teknolojia, ambaye alijiondoa baada ya kutopata kura nyingi Iowa na New Hampshire.

Alisifiwa kwa mchango wake katika midahalo na alionekana kuchangia kupunguza msukumo wa Marco Rubio.

Wakati wa kampeni, bw Christie alitetea sifa zake za kuwa mtu wa kufuata na kutekeleza sheria, akisema uzoefu wake alipokuwa afisa wa mashtaka baada ya mashambulio ya 9/11 unamuweka katika nafasi nzuri zaidi ya kulinda nchi hiyo dhidi ya magaidi.

Aidha, kama kiongozi wa Republican katika jimbo ambalo awali lilitawaliwa na wanachama wa Democratic, Bw Christie alisema alidhihirisha kwamba anaweza kufanya kazi na watu kutoka vyama vyote viwili.

Hata hivyo, msimamo wake kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, uhamiaji na haki za wapenzi wa jinsia moja uliegemea sana mrengo wa kulia na kumfanya kuwa kwenye kundi moja na wapinzani wake wahafidhina.

Bw Rubio alipanda kwenye kura baada ya kuandikisha matokeo mazuri Iowa. Lakini Christie alifanikiwa kumuonyesha kama mtu ambaye husita kufanya maamuzi muhimu.

Haki miliki ya picha ap
Image caption Christie (kulia) akishiriki mdahalo. Kushoto ni Ben Carson

Lakini wapinzani wengine wa Bw Christie, walioegemea msimamo wa wastani, gavana wa Ohio John Kasich na gavana wa zamani wa Florida Jeb Bush, wanaonekana kufaidi.

Mwaka 2012, viongozi wa Republican walikuwa wamemsihi Christie, aliyekuwa akivuma chamani, awanie urais lakini akakataa akisema hakuwa tayari.

Lakini alipojitosha ulingoni 2015, umaarufu wake ulikuwa umedidimia.