EU yaongeza ufadhili kwa uchaguzi Kenya

Uchaguzi
Image caption Uchaguzi mkuu Kenya umepangiwa kufanyika Agosti mwaka ujao

Umoja wa Ulaya umetoa euro milioni tano za kusaidia Kenya katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Kiasi hicho ni mara dufu ya kiasi kilichotolewa na umoja huo kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2013.

Balozi wa umoja huo nchini Kenya Bw Stefano Dejak amesema ustawi wa Kenya utategemea uthabiti wa kisiasa ambao una uhusiano wa moja kwa moja na uchaguzi.

Ufadhili huo utapitia kwa mfuko wa pamoja unaosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo (UNDP) wa kusaidia taasisi zinazohusika na uchaguzi Kenya.

"Uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika pamoja na mifumo thabiti ya uchaguzi huathiri hali ya maisha ya raia. Hili ni lengo letu la pamoja, kwamba mifumo ya uchaguzi inaboresha maisha ya wananchi na hasa wanawake, vijana na makundi yaliyotengwa,” amesema mwakilishi wa UNDP nchini Kenya Bw Michel Balima.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Kenya (IEBC) Ahmed Isaack Hassan aliyehudhuria hafla ya kutolewa kwa pesa hizo amesema tume inahitaji jumla ya Sh30 bilioni kuandaa uchaguzi huo wa mwaka ujao.

Ameiomba Hazina Kuu na Bunge kuhakikisha pesa hizo zinapatikana kwa wakati.

Tume hiyo inapanga kuanza shughuli kubwa ya kuwasajili wapiga kura Jumatatu wiki ijayo katika vituo 24,569 kote nchini.