Shule zafungwa Bangalore kwa sababu ya chui

chui Haki miliki ya picha Press Trust of India
Image caption India inakadiriwa kuwa chui karibu 14,000

Shule zaidi ya 100 zimefungwa nchini India baada ya chui mwingine kuripotiwa kuonekana viungani mwa mji wa Bangalore.

Wakazi wametakiwa kutotoka nje kwa sababu ya usalama wao. Polisi na maafisa wa misitu wanamsaka mnyama huyo.

Chui dume aliingia katika shule moja Jumapili na kuwajeruhi watu sita waliojaribu kumkamata.

Mwanasayansi na mfanyakazi wa idara ya misitu ni miongoni mwa waliojeruhiwa kwenye operesheni ya kumdhibiti mnyama huyo iliyodumu saa 10.

Chui wa sasa anadaiwa kuonekana na mfanyakazi wa ujenzi Jumatano eneo la Nallurhalli, karibu na Whitefield, mwandishi wa idhaa ya Kihindi ya BBC Imran Qureshi aliyeko Bangalore anasema.

"Tumeunga makundi ya maafisa wa misitu na polisi ambao wanazunguka eneo hilo wakimtafuta. Lakini kufikia sasa hatujaona dalili za kuwepo kwake,” afisa mkuu wa huduma za wanyamapori jimbo la Karnataka Ravi Ralph amesema.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Chui huyo alijeruhi watu sita shule ya Vibgyor Jumapili

Mnamo Alhamisi, serikali ya jimbo hilo iliagiza kufungwa kwa shule 129, zikiwemo 53 za serikali.

“Tutaamua baadaye jioni iwapo shule zitaendelea kufungwa Ijumaa au la. Tunasubiri uamuzi wa maafisa wa misitu na polisi,” afisa wa serikali KS Satyamurthy amesema.

Sensa ya karibuni zaidi ilionesha kuna karibu chui 14,000 nchini India.