Watu 8 wafa maji Nigeria

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu 8 wafa maji Nigeria

Watu 8 wamekufa maji Kaskazini mwa Nigeria baada ya mashua moja iliyokuwa ikisafirisha wafanyabiashara na abira kuzama.

Abiria waliokuwa kwenye mashua nyingine ndogo iliyokuwa karibu walijawa na wasi wasi na baadhi yao wanaripotiwa kujirusha majini ili wajinusuru.

Msemaji wa serikali ya mtaa katika eneo hilo Ibrahim Mu'azu ansema kuwa mashua ya kwanza ilikuwa ikisafirisha wachuuzi waliokuwa wakielekea katika soko moja iliyoko eneo la Jahun katika jimbo la Jigawa wakati ilipozama baada ya kugonga mwamba kwenye mto huo.

Amesema ajali hiyo iliwapa abiria wengine waliokuwa kwenye mashua nyingine wasi wasi mkuu, na baadhi yao walijirusha majini ili kuzuia mashua hiyo kuzama.

Kufika sasa miili ya watu wanane imepatikana kufuatia ajali hiyo iliyotokea jumatano.

Shughli ya kutafuta miili zaidi inaendelea na maafisa wa serikali wanasema hawajapata takwimu ya idadi kamili ya abiria waliokuwa kwenye mashua hizo.

Ajali za boti hutokea mara kwa mara nchini Nigeria, kwa sababu wamiliki wa mashua hizo hawazingatii sheria za usalama na mashua nyingi ziko katika hali mbaya.

Mwezi uliopita watu saba walifariki baada ya boti walimokuwa wakisafiria kuzama baada ya kugonga mwamba, katika mji wa bandari wa Lagos Kusini Magharibi mwa nchi hiyo.