Bangi: Waziri apendekeza wanafunzi wapimwe TZ

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bhangi: Waziri apendekeza wanafunzi wapimwe TZ

Waziri wa afya nchini Tanzania Ummy Mwalimu ametoa pendekezo kwa mkemia mkuu wa serikali kuanzisha utaratibu wa kuwapima wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kubaini iwapo wanatumia madawa ya kulevya.

Lengo la pendekezo hilo ni kujaribu kukabiliana na ongezeko la idadi ya vijana wanaojiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya hasa wanapokuwa mashuleni.

Ingawa haijulikani ni lini hasa pendekezo hilo litaanza kufanya kazi, lakini inaonyesha tatizo la vijana wanaojiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya ni kubwa nchini Tanzania.

Hofu zaidi iko kwa vijana hasa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao wanajihusisha na ulevi huo.

Waziri wa afya ameiambia BBC kwamba amewasilisha pendekezo hilo ili iwe ni kipaombele kwa ofisi ya mkemia mkuu kuwapima wanafunzi wote kama njia moja wapo ya kuthibiti matumizi ya madawa ya kulevya miongoni mwa vijana.

Waziri Ummy pia amemshauri mkemia mkuu kulifanyia majaribio pendekezo hilo katika maeneo yaliyoathirika zaidi nchini Tanzania kama vile Tanga, Dar es Salaam na Zanzibar.

Baadhi ya miji ndiyo inayotumika kuingizia madawa kama vile heroin, cocaine na mengineyo, hivyo kurahisisha upatikanaji wa madawa hayo.