Nyota mpya wa Instagram: Kutana na Hijarbie

Haki miliki ya picha Hijarbie

Ni wazo ambalo lilimjia Haneefah Adam alipokuwa akisomea shahada yake ya uzamili kuhusu nguvu za dawa – je, hali inawezakuwaje mwanasesere, maarufu kama Barbie, akivalishwa hijab?

“Niliona kulikuwa na pengo pahali. Sijawahi kuona mwanasesere amevalishwa hijab,” anasema mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 24, ambaye ni Mwislamu na huvalia hijab.

"Mwanzoni sikutaka kufanya lolote zaidi – nilitaka tu kupakia picha kwenye Instagram na sikudhani zingevutia watu.”

Haki miliki ya picha Hijarbie

Bi Adam alianza kuweka picha akitumia jina Hijarbie – na akaunti yake ikaanza kupata umaarufu.

Wiki chache baada ya kuweka picha yake ya kwanza, Bi Adam alianza kupongezwa na wanawake wengine wanaovalia hijab mtandaoni, ambao wanajiita “hijabis”.

Kutokana na hilo, watu wanafuata akaunti yake kwenye Instagram kwa sasa ni zaidi ya 31,000.

Bi Adam, anayetoka Ilorin nchini Nigeria, alishangazwa sana na kuvuma kwa picha zake.

“Watu wengi hawakuwa wameona kitu kama hiki kwengine na walipendezwa sana na wazo hili,” anasema.

“Wazazi wengi wanapendezwa na wazo hili pia kwani sasa watoto wao wanaweza kupata wanasesere wanaofanana nao.”

Haki miliki ya picha Hijarbie

Kutokana na umaarufu wa akaunti yake kwenye Instagram, Bi Adam sasa anaongeza picha anazopakia mtandaoni na anatumia muda mwingi katika kufuma na kushona.

“Huwa nashona nguo hizo mimi mwenyewe,” anasema.

Lakini kutengeneza wanasesere wadogo kuna changamoto zake.

“Inaweza kuchukua hadi saa mbili kutengeneza vazi kwani wanasesere hawa ni wadogo sana, lazima uwe makini.”

Haki miliki ya picha Hijarbie

Hata hivyo, wazo lake halijapokelewa vyema na kila mtu.

“Nilipoanza, watu wengi walitaka kununua wanasesere hawa, lakini pia imewafanya wengine kuanza kueneza chuki dhidi ya Waislamu,” anasema.

“Watu walikuwa wakifanyia mzaha mwanasesere huyo na kusema anabeba bomu.”

Bi Adam anatumai Hijarbie anaweza kukabiliana na dhana potofu kuhusu wanawake wanaovalia hijab.

“Kuna watu wanaofikiri msichana anayevalia hijab amekandamizwa na hilo si jambo wasichana wengi hufanya kwa hiari.

“Lakini hijab haisimamii dhuluma. Inahusu zaidi kukombolewa kwa wasichana na kuweza kujifunika.”

Haki miliki ya picha Hijarbie

Fashoni ya “Hijabi” imeanza kuvuma.

Mwaka uliopita, kampuni ya mavazi ya H&M ilizindua kampeni iliyoshirikisha mwanamke Mwislamu aliyevalia hijab.

Januari, kampuni ya mavazi na mitindo ya Dolce & Gabbana ilizindua mkusanyiko wa hijab ghali na za kifahari.

Je, hatima ya Hijarbie ni gani?

“Nilifungua akaunti ya Instagram kuwatia moyo wasichana Waislamu, ili wawe pia na mwanasesere wa kucheza naye anayefanana nao,” Bi Adam anasema.

Haki miliki ya picha Hijarbie

Anataka kutengeneza nguo nyingi na wanasesere na sanamu za maonyesho ya mavazi, na pia kuendelea kuandika mtandaoni kuhusu mavazi na mitindo.

“Ningependa sana kuendelea na akaunti hii ya Instagram.

“Lakini sijui kama itakuwepo miaka mitano ijayo.

“Lazima niwe makini zaidi na yale ninayopakia hapo, nazima niendelee kujaribu kutoa mchango wangu.”

Haki miliki ya picha Hijarbie