Wafungwa 49 wafariki Mexico

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gereza la Mexico

Mzozo kati ya makundi hasimu katika jela moja karibu na Monterrey kaskazini mwa Mexico umewaacha wafungwa 49 wakiwa wamefariki.

Gavana wa jimbo la Nuevo Leon Jaime Rodriguez amesema kuwa watu 12 walijeruhiwa katika gereza la Topo Chico baada ya wafungwa kupigana kwa kutumia vifaa hatari na fimbo.

Moto ulianzishwa katika ghala moja.

Maafisa wanasema hali imedhibitiwa na hakuna mfungwa aliyetoroka.Makundi ya jamaa za wafumngwa hao walifunga barabara wakitaka kupewa habari.

Baadhi yao walitupa fimbo na mawe na kujaribu kufungua lango la gereza hilo huku polisi wa kukabiliana na ghasia wakiwazuia.

''Hawajatuambia chochote,''alisema mama ya mfungwa mmoja ambaye alitaja jina lake kuwa Ernestina.

''Wamesema kuwa hadi watakapopata agizo '',hawataturuhusu ndani.Kila kitu hakiko sawa na hakuna mtu anayetufahamisha chochote''.

Kisa hicho kinajiri siku chache tu kabla ya ziara ya Papa Francis ambaye anatarajiwa kutembelea jela moja kaskazini mwa mji wa Ciudad Juarez,eneo linalojulikana sana kwa machafuko kati ya makundi ya biashara za mihadarati.