Rwanda kuwahamisha wakimbizi wa Burundi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Paul Kagame

Serikali ya Rwanda imetangaza kwamba itawahamisha mara moja wakimbizi wa Burundi hadi mataifa mengine.

Waziri wa maswala ya kigeni Luoise Mushikwabo amesema kuwa ukosefu wa maelewano haukubaliki ,baada ya mjumbe mmoja wa Marekani kuzungumzia kuhusu ripoti kwamba Rwanda imekuwa ikiwapa mafunzo wakimbizi wa Burundi ili kukabiliana na serikali ya Burundi.

Rwanda kwa sasa inawahifadhi makumi ya maelfu ya wakimbizi katika kambi.

Taarifa ya serikali imesema kuwa uwepo wao katika himaya yake,ikiwa ni karibu na taifa lao,ni hatari kwa wahusika wote.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wakimbizi wa Burundi

Wiki iliopita wataalam wa Umoja wa Mataifa waliliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa kwamba Rwanda imewasajili na kuwapa mafunzo wakimbizi kutoka Burundi wakiwemo watoto ambao walitaka kumuondoa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kutoka madarakani.

Burundi kwa mara kadhaa imeilaumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi walio na lengo la kuipindua serikali ya Bujumbura.

Hatahivyo Kigali imekana madai hayo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Pierre Nkurunziza

''Rwanda imechukua jukumu la kuwalinda na kuwaangalia wakimbizi'',ilisema taarifa ya serikali.

Hatahivyo imebainika katika eneo la maziwa makuu kwamba uwepo wao kwa kipindi cha mda mrefu karibu na taifa lao ni hatari kwa wahusika wote.

Taifa la Burundi limekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Nkurunziza kutangaza mipango mwezi Aprili kuwania muhula wa tatu,ambao alishinda.Mamia ya raia wameuawa na wengine 230,000 kulitoroka taifa hilo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maandamano ya Burundi

Rwanda inawahifadhi zaidi ya wakimbizi 70,000 ikiwemo 24,000 wanaoitwa wakimbizi wa mijini.Kambi kubwa ya wakimbizi nchini humo ni ile ya Mahama.

Hakuna kambi nyengine zozote za wakimbizi zinazojulikana isipokuwa kambi ndogo za muda kwa wale wanaongojea kupelekwa katika kambi ya Mahama.