Jamhuri ya Afrika ya Kati wapiga kura

Haki miliki ya picha

Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamepiga kura kumchagua rais mpya katika uchaguzi unaorudiwa baina ya waliokuwa mawaziri wakuu, Faustin Touadera na Anicet Dologuele.

Pia watachagua wabunge baada ya uchaguzi uliofanywa mwezi Disemba mwaka jana kubatilishwa kutokana na kasoro zilizojitokeza.

Mwandishi wa BBC Abdourahmane Dia kutoka Bangui anasema mara hii, wananchi hawakuwa na hamasa kubwa ya kupiga kura, ingawa maafisa wa tume ya uchaguzi wanasema upigaji kura umefanyika vizuri.

Wapiga kura wanachagua rais wao na wabunge wao katika uchaguzi ambao unatarajiwa kumaliza mapigano ya zaidi miaka mitatu baina ya jamii za nchi hiyo.

Hakuna matukio makubwa yaliyoshuhudiwa, lakini vituo vya kupigia kura vilionekana vikiwa na wapiga kura wachache, ikilinganishwa na uchaguzi uliofanyika mara ya kwanza, hayo ni kwa mujibu wa mwandishi wa BBC ambae yuko katika mji mkuu wa Bangui.

Tatizo la mipango na ukosefu wa baadhi ya vifaa umetawala uchaguzi huo kama walivyoeleza baadhi ya wapiga kura.

"nimeshindwa kupiga kura kwa sababu jina langu halipo katika daftari la kupiga kura. Na mara ya mwisho niliweza kupiga kura, lakini leo wamekataa. Inaumiza, ni uonevu kwa sababu mimi ni raia pia."

"nimeshindwa kuona jina langu na mara ya mwisho nimepiga kura hapa. Nimeangalia kila sehemu lakini sijaona jina langu. Sijui nitafanya nini sasa."

Hata hivyo, maafisa wa tume ya uchaguzi wamesema kwamba hatua mpya zimechukuliwa ili kuepusha mapungufu hayo.

Marudio ya uchaguzi huo yanafanyika mwezi mmoja na nusu baada ya mchuano wa mara ya kwanza ambapo wagombea thelathini waliingia kwenye kinyang'anyiro cha urais.

Wagombea wote wawili Anicet Dologuele, ambae amebobea katika maswala ya benk na Faustin Touadera, ambae ni mhadhiri wa chuo kikuu, wote wanasimamia umoja wa kitaifa, usalama, na uchumi.

Hata hivyo, atakaeibuka kidedea, atatakiwa haraka sana, atatue tatizo la makundi yenye kumiliki silaha ambayo bado yana nguvu katika maeneo mbali mbali ya nchi licha ya kuwepo kwa vikosi vya kulinda amani elfu kumi na moja vya Umoja wa Mataifa.