Milipuko ya guruneti yatikisa Burundi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Milipuko ya guruneti yatikisa Burundi

Mvulana mmoja mwenye umri a miaka 11, ameuwawa kwenye moja kati ya mashambulio manne ya maguruneti, yaliyotikiza mji mkuu wa Burundi, Bujumbura leo asubuhi.

Watu zaidi ya 30 wamejeruhiwa wakiwemo wanawake na watoto.

Waziri wa usalama wa taifa wa Burundi, ameyataja mashambulio hayo kuwa ni visa vya ugaidi.

Mashambulizi sawa na hayo yalitekelezwa wiki iliyopita na kuwaacha wengi na majeraha.

Mlipuko wa kwanza wa grenedi uliskika dakika chache baada ya saa mbili asubuhi, katika kituo cha kuuzia petroli katikati mwa mji mkuu.

Watu wanane walijeruhiwa hapo.

Mlipuko mwingine ulifuata, kwa karibu mno na milipuko zaidi katika maeneo tano tofauti, likiwemo eneo lililo karibu na soko maarufu, ambapo mtoto mmoja aliuwawa na watu kadhaa kujeruhiwa.

Image caption Waziri wa usalama wa taifa wa Burundi, ameyataja mashambulio hayo kuwa ni visa vya ugaidi.

Shambulizi la leo linajumlisha idadi ya watu waliouwawa kwa muda wa wiki mbili zilizopita kuwa 8 na wengine 100 kujeruhiwa.

Hakuna kundi lililokiri kutekeleza mashambulizi hayo yanayoonekana kuwa yalipangwa.

Makundi kadhaa ya wapiganaji yameibuka katika kipindi cha majuma kadhaa yaliopita.

Kulingana na umoja wa mataifa, zaidi ya watu 430 wameuwawa, tangu rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania urais kwa muhula wa tatu mwezi Aprili mwaka ulopita.