HRW: Waliobakwa Kenya wametelekezwa

Wanawake Haki miliki ya picha Samer Muscati Human Rights Watch
Image caption Visa 900 vya ubakaji viliripotiwa wakati ghasia hizo 2007/2008

Ripoti mpya ambayo imetolewa na shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch nchini Kenya inadai kwamba wanawake na wasichana waliobakwa wakati wa vurugu za baada ya uchaguzi wa 2007, bado wanakabiliwa na matatizo ya kimwili, kiafya na kisaikologia.

Pia ripoti hiyo inasema serikali ya Kenya haijakuwa ikitoa usaidizi wa kimsingi kuwasaidia waathiriwa hao.

Shirika hilo la kutetea haki za kibinadamu limegundua kwamba waathiriwa wengi waliohojiwa wanahitaji matibabu.

Hali hii imesababisha wengi wao kotoweza kumaliza masomo ama kufanya kazi huku wakiishi kwa umaskini na njaa.

Hivi karibuni, serikali ya Kenya ilizindua mradi wa kutoa msaada kwa wale walioathirika wakati wa ghasia hizo za baada ya uchaguzi wa 2007/2008 nchini Kenya, wanufaika wakiwemo wale waliodhalalishwa kingono.

Ghasia hizo za baada ya uchaguzi zilisabababisha vifo vya watu 1,133 huku watu zaidi ya 600,000 wakikimbia makwao.

Kulingana na ripoti hiyo, zaidi ya visa 900 vya ubakaji viliripotiwa.

BBC imezungumza na mmoja ya waathiriwa, Bi Elizabeth Atieno, ambaye kwa sasa anaishi katika mtaa wa mabanda wa Mathare jijini Nairobi.

Image caption Bi Atieno alitengwa na familia yake

Elizabeth alijipata katikati ya vurugu, ambapo wanaume waliojahami kwa silaha walimshambulia na kumbaka.

"Upigaji kura ulipoanza, sikuwa mtu wa siasa mimi, sikuweza kubashiri kama kutakuwa na vurugu, na wakati matokeo yalipotangazwa, nilikuwa nikirejea nyumbani kutoka kwa shangazi yangu, nilikutana na genge la wanaumme, walishambulia kwa kunipiga, wakanibaka na hivyo ndivyo ilifanyika," anasema.

Na ni hapo ndipo mambo yalianza kumuendea mrama Elizabeth.

Kuongeza shida juu ya shida, alipata mimba kutokana na kitendo hicho cha ubakaji na familia yake ikamsaliti

"Kila mtu alitaka niavye mimba, hivo ndivyo familia yangu ilitaka, hakuna yeyote alitaka kunisaidia na matibabu, kwa hivyo mimi nilichoka na kukimbia nyumbani."

Elizabeth alipotoroka nyumbani, hapo ndipo alijapata katika mtaa wa mabanda wa Mathare, unaopatikana viungani mwa mji mkuu wa Nairobi, katika hali ya upweke, umaskini na maisha magumu.

Lakini kwake sasa, haya maisha huyana budi ila kuishi. Huwa anaishi katika chumba kimoja kilichojengwa kwa udongo.

Miaka minane baadaye, alijaliwa kupata mume, na kujenga familia.

Lakini ni nini hasa msukumo wake wa kujistahimili

Huwezi kusikiliza tena

"Nilijaliwa mtoto na kumuita Brooklyn, kumtunza na kumlea mtoto kama huyo si rahisi, hasa kama hauna anayekusaidia. Unajua kwa nini niko huru? Ni kwa sababu nampenda Brooklyn, kwa sababu Brooklyn ndiye malaika wangu, kila hatua ninayochukua, huwa namwaza sana."

Miaka inapozidi kwenda, Elizabeth anazidi kupata nguvu kila siku hasa kwa kujihusisha katika mifumo ya kuwahammsisha wanawake dhidi kuhusu dhuluma za kijinsia

"Siku za usoni, natarajiwa kuwa na jukwaa, hapa Kenya na kimataifa, la kuwapa wanawake nguvu kwa sababu, watu hawajui kwamba ubakaji hutokea. Mwili wa mwanamke si uwanja wa vita, ambapo unautumia kumaliza hasira zako.”

Anapoendelea kuosha vyombo akijiandaa kuanza siku, simulizi ya aliyopitia inaashiria haja kuu ya uhamasisho kuhusu masuala ya jinsia, wanawake na mtoto wa kike na pia waathiriwa wa dhuluma na unyanyasaji.