Kanye West aomba pesa kutoka kwa Zuckerberg

Kanye West Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kanye West alisema majuzi kwamba anadaiwa $53m

Mwanamuziki Kanye West amemuomba hadharani mwaanzilishi wa Facebook Mark Zuckerberg ampe usaidizi wa kifedha.

West anataka Zuckerberg awekeze $1bn (£700m) katika miradi yake akisema yeye binafsi hana “rasilimali za kutosha” kuunda kile ambacho “anaweza”.

Ametoa ombi hilo siku chache tu baada ya kutangaza kwamba ana deni la $53m (£36m) alipokuwa akitoa albamu yake mpya.

West alijitetea kupitia msururu wa jumbe kwenye Twitter.

Waandishi wa BBC Newsbeat wamewasiliana na maafisa wa Facebook ambao wamesema: “Hatuna lolote la kusema kwa sasa.”

Jambo la kushangaza ni kwamba Kanye West amemuomba Zuckerberg usaidizi kupitia Twitter ambao ni mtandao unaoshindana na Facebook.