Rais wa Pakistan ashutumu Siku ya Valentino

Valentino Haki miliki ya picha Getty
Image caption Siku ya Wapendanao huadhimisha kila 14 Februari

Rais Pakistan ameshutumu maadhimisho ya Siku ya Wapendanao na kusema siku hiyo haina uhusiano wowote na utamaduni wa Pakistan na haifai kuadhimishwa.

Rais Mamnoon Hussain aliwaambia wanafunzi kwamba huo ni “utamaduni wa Magharibi” na unaenda kinyume na utamaduni wa Kiislamu.

Alitamka hayo baada ya wilaya moja kaskazini magharibi mwa nchi hiyo kupiga marufuku sherehe za kuandimisha Siku ya Wapendanao ambao pia hujulikana kama Siku ya Valentino.

Siku hiyo huadhimishwa katika maeneo mengi duniani kila tarehe 14 Februari.

Huwa maarufu sana katika miji mingi Pakistan lakini makundi ya kidini yameishutumu na kusema ni uozo kimaadili.

Mapema wiki iliyopita serikali ya mji wa Kohat, jimbo Khyber Pakhtunkhwa, iliwaagiza polisi kuzuia maduka kuuza kadi za Valentino na bidhaa nyingine.

Baraza la mji wa Peshawar pia liliidhinisha azimio la kupiga marufuku sherehe za kuadhimisha siku hiyo likisema ni “siku isiyo na manufaa yoyote”.