Waliohusishwa na ugaidi Ethiopia waachiliwa

Image caption Maandamano ya kupinga kukamatwa kwa wanaharakati nchini Ethiopia

Wanasiasa wawili wa upinzani nchini Ethiopia wamewachiliwa huru jijini Addis Ababa, miezi kadhaa baada ya kukamatwa kwa madai ya kuhusika na ugaidi.

Habtamu Ayalew na Abraham Solomon wamekuwa gerezani tangu July 2014, licha ya mahakama kufutilia mbali mashtaka dhidi yao mwaka uliopita.

Habtamu ambaye ni mkosoaji mkubwa wa seikali na Abraham, ambaye ni mwanaharakati na mwalimu walikamatwa mwaka wa 2014 na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria tata ya kukabiliana na ugaidi nchini humo.

Lakini mahakama jijini Addis Ababa ilifutilia mbali mashtaka hayo kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha na kuamuru kuwachiliwa kwa wawili hao.

Hata hivyo walisalia kizuizini baada ya upande wa mashtaka kukata rufaa.

Kesi hiyo ya rufaa bado inaendelea. Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuwa wanachama wa Ginbot 7, chama cha kisiasa ambacho kimepigwa marufuku nchini Ethiopia na ambacho serikali inasema ni cha kigaidi.

Shirika la kutetea haki za Kibinadamu la Human Rights watch limepongeza hatua ya kuwachiliwa huru kwa wawili hao, lakini likashtumu kuendelea kuhangaishwa kwa upinzani.

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Ethiopia wamekuwa wakiishtumu serikali mara kwa mara, kuwa inatumia sheria tata dhidi ya ugaidi, kuwahangaisha wapinzani, na kukandamiza uhuru wa kujieleza.

Wanasiasa kadha wa upinzani wamekamatwa huku wengine wakitoroka nchi hiyo kwa kuhofia maisha yao.

Katika uchaguzi uliopita, chama kinachotawala kilishinda viti vyote vya ubunge na kuiwacha nchi hiyo bila mwakilishi wowote wa upinzani katika bunge.