Tume ya uchaguzi Uganda yaahidi uchaguzi huru

Kura Haki miliki ya picha Electoral Commission of Uganda
Image caption Watu wataanza kupiga kura saa moja asubuhi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Uganda imeahidi kwamba imejiandaa vya kutosha kuzima udanganyifu wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho.

Mwenyekiti wa tume hiyo Bw Badru Kiggundu amesema: "Bahasha za kubeba matokeo ya kura haziwezi kufunguliwa bila sisi kujua. Ukizifungua wakati matokeo yanasafirishwa, tutajua.”

Kuna ripoti kwamba kuna watu wanaochapisha karatasi bandia za kura za urais na Bw Kiggundu amewataka raia kuwa macho.

Amewaomba wanasiasa kutounda makundi ya kulinda kura akisema ni polisi pekee walio na jukumu la kudumisha amani na utulivu vituoni.

Upigaji kura utaanza saa moja asubuhi na kumalizika saa kumi alasiri.

Wapiga kura watakaokuwa kwenye foleni saa kumi alasiri wataruhusiwa kupiga kura.

Bw Kiggundu amewahimiza wapiga kura kufika vituoni mapema.

Ameahidi kwamba matokeo yatajulikana katika kipindi cha saa 48.

Wakati wa kupiga kura, kutakuwa na nambari maalum ya simu ambayo itatumiwa na tume hiyo kupokea malalamiko kutoka kwa wapiga kura.

Kuna wapiga kura 15 milioni ambao watakuwa wakiamua kati ya wagombea wanane ni nani anafaa kuongoza taifa hilo kwa muhula mwingine wa miaka mitano.