Kerry amlalamikia Museveni kuhusu uchaguzi

Besigye
Image caption Besigye amekamatwa na polisi mara tatu wiki hii

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry amezungumza kwa simu na Rais Yoweri Museveni na kueleza wasiwasi wake kuhusiana na kukamatwa mara kwa mara kwa mgombea urais wa FDC Kizza Besigye.

Amemtaka Rais Museveni kuwadhibiti polisi na maafisa wengine wa usalama.

Bw Kerry pia amekosoa hatua ya serikali ya kufunga mitandao ya kijamii na kutoa wito kwa Rais Museveni kuagiza mitandao hiyo ifunguliwe mara moja.

Image caption Polisi wamekuwa wakishika doria maeneo mengi ya Kampala

Waziri huyo amemwambia Bw Museveni kwamba kukamatwa kwa Dkt Besigye na kuhangaishwa kwa wanachama wa upinzani wakati wa upigaji kura na kuhesabu kura „kunatilia shaka kujitolea kwa Uganda katika kuhakikisha uchaguzi huru, wazi na wa kuaminika.”

Dkt Besigye amekamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa polisi mara tatu wiki hii. Mara ya kwanza ilikuwa Jumatatu akielekea mkutano wa kampeni Kampala.

Haki miliki ya picha AP

Alikamatwa tena jioni siku ya uchaguzi Alhamisi na Ijumaa tena akakamatwa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bw Kerry

”Ustawi wa Uganda utategemea kuheshimu maadili ya demokrasia katika uchaguzi unaoendelea. Marekani iko pamoja na watu wa Uganda wakishiriki shughuli hii muhimu ya kidemokrasia,” Bw Kerry amemwambia Bw Museveni, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Marekani.

Hata hivyo, waziri huyo wa Marekani amefurahishwa na hatua ya Tume ya Uchaguzi kuchukua hatua na kuongeza muda wa kupiga kura katika maeneo ambayo upigaji kura ulitatizika siku ya kwanza.