Simba watoroka mbuga na kuingia mtaani Nairobi

Image caption Simba watoroka mbuga ya wanyamapori Kenya

Simba wanne wametoroka mbuga ya taifa ya wanyamapori ya Nairobi. Taarifa zinasema mara ya mwisho walionekana eneo la makazi la Langata.

Tayari shirika la wanyama pori la Kenya KWS limeanzisha oparesheni ya kuwasaka wanyama hao.

Shirika hilo limewataka wakaazi wa maeneo hayo kutahadhari.

Hii si mara ya kwanza kwa wanyama hao kuzua taharuki katika eneo hilo.

Msemaji wa Shirika hilo Paul Udoto ameambia BBC nchini Kenya kwamba wamepokea habari kwamba simba hao wa kike walionekana katika nyumba za NHC katika eneo la Langata na mitaa mengine inayopakana na Barabara ya kusini.

''Haya ni maeneo ambayo yana watu wengi, na hii ndio maana tumeimarisha msako wetu,'' aliambia BBC kwa njia ya simu, yeyote aliye na habari kuwahusu anapaswa kutoa habari hizo mara moja.

''Kikosi chetu kikishirikiana na madaktari wa wanyama kimeenda eneo la Langata kuwasaka wanyama hao tangu saa kumi na moja asubuhi,'' aliongezea.

Shirika la KWS limesema simba hao walitoweka kutoka mbuga hiyo wiki moja iliyopita lakini ni usiku wa kuamkia leo ambapo ripoti za kuonekana kwao ziliripotiwa.

Langata ni eneo lililo na watu wengi na maafisa wa KWS pamoja na polisi wanahofia kwamba wanyama hao huenda wakasababisha hasara iwapo hawatapatikana haraka na kurudishwa katika mbuga hiyo.

Simba sita waliripotiwa kutoroka katika mbuga hiyo Alhamisi jioni lakini wanne kati yao walipatikana .