Donald Trump amsifu Papa Francis

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Papa Francis na Donald Trump

Mgombea wa urais wa chama cha Republican Donald Trump amempongeza kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis, saa kadhaa baada ya kiongozi huyo wa dini kutilia shaka kuhusu imani yake ya kidini.

Papa alikuwa amesema kuwa pendekezo la bwana Trump la kuunda ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico si la mtu mwenye imani ya dini ya kikristo, hatua iliosababisha hisia kali kutoka kwa mfanyibiashara huyo.

Lakini saa kadhaa baadaye, katika ukumbi mmoja kusini mwa mji wa Carolina,bilionea huyo ambaye ni mwekezaji mkubwa wa hoteli alikuwa na sauti ya maridhiano.

Wapiga kura wa chama cha Republican watamchagua ni nani atakayewawakilisha katika tiketi ya kugombea urais ya chama hicho siku chache zijazo.

Bwana Trump anaongoza kura ya jimbo la Carolina Kusini na alikuwa katika runinga ya kitaifa katika eneo la Columbia kujibu maswali.

Na alipoulizwa kuhusu mgogoro wake na papa Francis,alisema kwamba hawezi kuuelezea kama vita,ijapokuwa alisema baadaye kwamba asingependa kutofautiana na Kiongozi huyo wa dini.