Museveni: Uchaguzi wa Uganda ulikuwa shwari

Huwezi kusikiliza tena

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema uchaguzi uliofanyika nchini humo Alhamisi wiki iliyopita ulikuwa wa haki na akasema wanaoutilia shaka “hawaielewi Uganda.”

Aidha, ametetea hatua ya maafisa wa usalama kumzuilia mgombea mkuu wa upinzani Dkt Kizza Besigye wa chama cha FDC.

Tume ya Uchaguzi ilisema Jumapili kwamba Bw Museveni alipata ushindi wa asilimia 60.75 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Dkt Besigye aliyepata asilimia 37.35.

Upinzani umedai kuwepo wizi wa kura na waangalizi wa kimataifa wamesema pia kwamba hakukuwa na nafasi sawa ya ushindani.

Waangalizi hao wamelalamikia kukamatwa na kuzuiliwa kwa Dkt Besigye, kucheleweshwa kwa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura na kuzimwa kwa mitandao ya kijamii.

Mkuu wa waangalizi wa Jumuiya ya Madola, Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, alisema matatizo mengi katika utaratibu wa uchaguzi yalitia dosari uaminifu na uhaki wa shughuli nzima

Lakini Bw Museveni amesema hataki ukosoaji kutoka nje.

Akizungumza na mwandishi wa BBC Zuhura Yunus, katika mahojiano maalum Nyumbani kwake Rwakitura Magharibi mwa Uganda Museveni, Bw Museveni alisema waangalizi hao hawaelewi vyema taifa la Uganda.

Image caption Bw Museveni amesema polisi na wanajeshi walitumwa mijini kuzuia fujo

"Maafisa wa usalama walikuwa wengi kulinda usalama. Kwa sababu walikuwa wanataka kufanya fujo. Wajua wapinzani wa hapa sio kama wa Ulaya. Hawajaiva kisiasa. Usipokuwa mwangalifu wanaweza kuleta fujo kabisa. Na sisi hatuwezi kukubali hivyo,” amesema.

Kuhusu kukamatwa na baadaye kuzuiliwa kwa Dkt Besigye nyumbani kwake, Rais Museveni alisema kiongozi huyo alikuwa amepanga kujitangazia matokeo yake jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

"Walikuwa wanataka kufanya fujo. Kwanza walikuwa wanataka kutangaza matokeo yao, wenyewe ya uongo. Pili walitaka kufanya fujo za kuharibu mali,” amesema.

"Tulitaka kuwawahi hawa wafanya fujo na ndio sababu polisi iliwazuia. Sasa uchaguzi umekwisha, mipango yao tumeivunja, basi tunawaacha. Hatuna shida nyingine nao.”

Bw Museveni ambaye sasa ana umri wa miaka 71 anatarajiwa kufikisha umri wa kustaafu wa miaka 75 akikaribia kumaliza muhula wa sasa.

Amesema hana mipango ya kufanyia marekebisho katiba ili kuendelea kuongoza taifa hilo.

"Hakuna mpango wowote. Hatujazungumzia hilo. Lilikuja kwenye baraza la mawaziri tukasema hapana, hakuna haja ya kuongeza.”