Rubani adaiwa kumdhalilisha polisi wa kike Kenya

Rubani
Image caption Bw Boinnet amemtaka rubani huyo kujisalimisha kwa polisi

Polisi nchini Kenya wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa ambapo rubani wa ndege iliyombeba Naibu Rais William Ruto anadaiwa kumdhalilisha afisa wa polisi wa kike.

Kisa hicho kilitokea Jumapili wakati Bw Ruto alikuwa amezuru mji wa Ndunyu Njeru, jimbo la Nyandarua katikati mwa nchi hiyo.

Video iliyochukuliwa na mmoja wa walioshuhudia kisa hicho imesambaa sana mtandaoni watu wakitaka hatua zichukuliwe dhidi ya rubani huyo.

Kwenye video hiyo, rubani huyo anaonekana akimkaripia mwanamke huyo ambaye wakati huo anatumia simu, kumpokonya bakora yake na kisha majibizano yanatokea. Muda mfupi baadaye, rubani huyo anaonekana akimsukuma afisa huyo wa polisi.

Image caption Watetezi wa haki wameshutumu kisa hicho

Mkuu wa polisi Joseph Boinnet, kupitia taarifa, ameagiza maafisa wa polisi kuanzisha uchunguzi mara moja kuhusu kisa hicho na pia akamtaka rubani huyo kujisalimisha kwa polisi.

Afisa wa mawasiliano wa Bw Ruto, Bw David Mugonyi, amesema kiongozi huyo amefahamishwa kuhusu kisa hicho.

Haki miliki ya picha Citizen TV Kenya RMS
Image caption Msemaji wa Bw Ruto ameshutumu kisa hicho

“Naibu Rais amewaagiza polisi kuchukua hatua mara moja. Naibu Rais anaheshimu polisi wetu wenye bidii ambao hufanya kazi saa nyingi kulinda nchi. Kisa hiki hakikubaliki, na ni cha kusikitisha na nimewataka polisi kuchunguza kitendo hicho cha rubani huyo,” taarifa yake imesema.