Chifu amnajisi msichana 13 Nigeria

Haki miliki ya picha Kwa hisani
Image caption Mkuu wa jimbo la Kano, Muhammadu Sanusi wa pili, amemsimamisha chifu huyo kazi kwa muda

Kiongozi mmoja wa jamii Goron Maje kaskazini mwa Nigeria amesimamishwa kazi kwa kumnajisi msichana mwenye umri wa miaka 13 na kumuambukiza virusi vya ukimwi.

Chifu huyo Musa Muhammad, ambaye ndiye anayesimamia kijiji cha Goron Maje iliyoko katika wilaya ya Dambatta alikamatwa baada ya wazazi wa msichana huyo kupiga ripoti kuwa mwana wao alikuwa ametendewa unyama huo na kiongozi huyo.

Kiongozi wa kidini katika jamii hiyo aliwakata maini wazazi wa msichana huyo alipowaambia kuwa uchunguzi wa kimsingi katika hospitali ya kijiji hicho ulibaini kuwa alikuwa ameambukizwa virusi vya ukimwi.

Mkuu wa jimbo la Kano, Muhammadu Sanusi wa pili, amemsimamisha kazi kwa muda, huku uchunguzi wa kisa hicho ukiendelea.

kumekuwa na ongezeko la visa vya ubakaji na dhulma dhidi ya watoto wa kike katika jimbo la Kano ila tukio hili limepata umaarufu mkubwa kwa sababu aliyetekeleza makosa hayo ndiye anayestahili kuwalinda watoto wa kike.

Bwana Muhammad hajasema lolote kuhusu tuhuma zinazomkabili.