Ndege iliyowabeba watu 23 yatoweka Nepal

Ndege Haki miliki ya picha EPA
Image caption Maafisa wa uokoaji wamepata mabaki ya ndege hiyo

Ndege ndogo iliyowabeba watu 23 imetoweka ikiwa maeneo yenye milima nchini magharibi mwa Nepal.

Ripoti zinasema mabaki ya ndege hiyo yamepatikana ingawa hakuna habari kuhusu majeruhi au manusura.

Ndege hiyo ilikuwa safarini kutoka Pokhara, magharibi mwa mji mkuu Kathmandu, kwenda Jomsom, eneo ambalo watu wengi wanaoenda kukwea milima ya Himalaya huanza safari yao ya kukwea milima hiyo.

Ndege hiyo ilipoteza mawasiliano na maafisa wa udhibiti wa safari za ndege wa Pokhara dakika 10 baada ya kupaa.

Hakuna viwanja vya ndege kati ya maeneo hayo mawili na inahofiwa kwamba ndege hiyo imeanguka.

Haki miliki ya picha

Maafisa wanasema ndege hiyo ya shirika la Tara Airlines ilikuwa na marubani watatu na abiria 20, mmoja wao raia wa Uchina na mwingine wa Kuwait. Wawili kati ya abiria waliokuwa wamebebwa na ndege hiyo walikuwa watoto.

Ajali za ndege hutokea mara kwa mara nchini Nepal.

Tangu mwaka 1949, kumetokea zaidi ya ajali 70 zilizohusisha ndege za kawaida na helikopta, na vifo vya watu 700.