Watoto 2 wamshtaki TB Joshua kwa kifo cha baba yao

Ajali ya kanisa
Image caption Watu zaidi ya 100, wengi wao kutoka Afrika kusini walikufa wakati jengo la kanisa la Muhubiri TB Joshua lilipoporomoka,

Watoto wawili wa Afrika Kusini wanamshitaki mhubiri wa kanisa kubwa na maarufu nchini Nigeria TB Joshua kwa kifo cha baba yao, wakili wao Bolajii Ayorinde ameiambia BBC.

Watoto hao mmoja mwenye umri wa miaka mitatu na mwingine wa miaka sita wamewasilisha nyaraka za mashtaka katika mahakama ya mji mkuu wa Nigeria, Lagos, wakidai fidia ya zaidi ya dola $521,000 kutoka kanisa la Synagogue Church of All Nations, vyombo vya habari vya Nigeria vimeripoti.

Image caption Muhubiri TB Joshua na kanisa lake wamekuwa wakisisitiza kwamba hawana kosa lolote

Baba yao alikuwa miongoni mwa watu 116 waliokufa wakati jengo la makazi yanayomilikiwa na kanisa hilo lilipoporomoka mjini Lagos mwaka 2014.

Mwaka jana mahakama ya uchunguzi wa vifo iliamuru TB Joshua anapaswa kushtakiwa juu ya kuporomoka kwa jengo, akisema kanisa hilo linahusika kwasababu ya uzembe wa kiuhalifu. Muhubiri TB Joshua na kanisa lake wamekua wakikana kufanya kosa lolote.