Gianni Infantino ndio rais mpya wa Fifa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Gianni Infantino ndiye aliyechaguliwa kuwa rais mpya wa shirikisho la soka duniani Fifa

Raia wa Switzerland Gianni Infantino amechukua mahala pake Sepp Blatter kama rais wa shirikisho la soka duniani Fifa.

katibu huyo mkuu wa Fifa alipata kura 115 katika raundi ya pili ikiwa ni kura 27 zaidi ya mpinzani wake wa karibu Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa.

Mwanamfalme Ali bin al-Hussein alikuwa wa tatu akiwa na kura nne huku Jerome Champagne akishindwa kupata hata kura moja.

Tokyo Sexwale alijiondoa kabla ya kura kuanza kupigwa mjini Zurich.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Infantino

Raundi ya kwanza ya upigaji kura ilishindwa kum'baini mshindi wa moja kwa moja.

Wingi wowote wa kura[zaidi ya aslimia 50] katika raundi ya pili ya uchaguzi huo ulikuwa unaweza kumwezesha mgombea kutangazwa mshindi katika raundi ya pili.

Infantino ni wakili mwenye umri wa miaka 45 kutoka eneo la Brig jimbo la Valais nchini Switzerland ,ikiwa ni eneo lililopo chini ya maili sita kutoka nyumbani kwa Blatter.

Blatter ambaye aliliongoza shirikisho hilo tangu mwaka 1998 alijiondoa mwaka uliopita kabla ya kupigwa marufuku katika shughuli zozote za kandanda kwa kipindi cha miaka sita .

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Infantino akiwahutubia wajumbe

Baada ya kutangazwa mshindi, Infantino aliwaambia wajumbe waliopiga kura kwamba hakuweza kujielezea kutokana na hisia alizokuwa nazo.

Lakini aliwaambia wajumbe kwamba ''kwa pamoja wataweza kuirudisha sura ya Fifa na heshima ya Fifa''.