Leonardo DiCaprio ajishindia tuzo ya Oscar

Brie Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Brie Larson ameshinda tuzo ya mwigizaji bora wa kike naye DiCaprio mwigizaji bora wa kiume

Mwigizaji nyota Leonardo DiCaprio hatimaye amejishindia tuzo yake ya kwanza ya Oscar kwa uigizaji wake katika filamu ya The Revenant, baada ya kushindania tuzo hizo mara sita.

Ametawazwa mwigizaji bora kwenye makala ya 88 ya tuzo hiyo.

Tuzo ya mwigizaji bora wa kike imemwendea Brie Larson kwa uigizaji wake katika filamu ya Room.

Spotlight ndiyo iliyozoa tuzo ya filamu bora zaidi Oscar ingawa filamu Mad Max: Fury Road ndiyo imezoa tuzo nyingi, ikichota tuzo sita.

Mark Rylance ameshinda tuzo ya mwigizaji bora msaidizi katika tuzo hizo za Oscars, huku Miwngereza mwenzake Sam Smith akishinda tuzo ya wimbo bora asilia original song.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Leonardo DiCaprio ameshangiliwa sana akipokea tuzo

Miongoni mwa walioshindia Mad Max: Fury Road, iliyokuwa imeteuliwa kushinda tuzo kumi, ni mbunifu Mwingereza Jenny Beavan, aliyeshinda tuzo ya ubunifu wa mavazi bora zaidi.

Filamu ya The Revenant imeshinda tuzo tatu kati ya 12 ilizoteuliwa kupigania.

Alejandro Inarritu amezoa tuzo ya mwelekezi bora naye Emmanuel Lubezki akajishindia tuzo yake ya tatu mtawalia ya Oscar katika kuandaa sinema bora, baada ya kushinda kwa filamu ya Birdman 2015 na Gravity 2014.

DiCaprio ameshangiliwa sana akienda kupokea tuzo yake. Alikuwa ameteuliwa kupigania tuzo hiyo mara sita awali, tano kama mwigizaji bora na moja kama produsa wa filamu ya Wolf of Wall Street lakini hakufanikiwa kushinda.

Alisema filamu ya The Revenant ilikuwa "kuhusu uhusiano wa binadamu maumbile asilia.”

"Mabadiliko ya tabia nchi ni jambo la kweli, mabadiliko haya yanafanyika,” amesema.

"Ndilo tishio kubwa zaidi kwa sasa kwa viumbe wote na tunahitaji kuchukua hatua sasa.”