Mamia wauawa Nigeria katika wizi wa mifugo

Haki miliki ya picha State House
Image caption Rais wa Nigeria ameamrisha uchunguzi ufanyike kuhusu wizi wa mifugo

Rais wa Nigeria ameamrisha uchunguzi ufanyike kuhusu ghasia zilizozuka kufuatia wizi wa mifugo uliosababisha vifo vya mamia ya watu juma lililopita.

Katika taarifa yake rais Muhammadu Buhari amesema ameshutushwa sana na ghasia hizo katika jimbo la kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Buhari ametoa amri hiyo kwa walinda usalama wake kutafuta chanzo cha matatizo hayo, kufuatia misururu ya mashambulio katika vijiji kadhaa.

Image caption Mamia wauawa Nigeria katika wizi wa mifugo Benue

Vyombo vya habari nchini humo, vimeripoti kwamba baadhi ya vijiji viliteketezwa kabisa, na kulazimisha idadi kubwa ya watu kukimbia maskani yao.

Kumekuwa na wito kutoka kwa wanasiasa wa maeneo hayo kutuma jeshi ili kuleta utulivu.

Jimbo la Benue, lina historia ya ghasia mbaya na mashambulio ya mara kwa mara kati ya jamii ya wafugaji na wakulima - hasa wakigombania mahala pa kulishia mifugo wao, jambo linalosababisha wizi mkubwa wa mifugo.

Image caption Mashambulio hayo ya hivi punde ya wizi wa mifugo ni changamoto lingine kwa serikali ya rais Muhamadu Buhari inayosumbuka na Boko Haram

Mashambulio hayo ya hivi punde ya wizi wa mifugo ni changamoto lingine kwa serikali ya rais Muhamadu Buhari.

Utawala wa Nigeria ungali unakabiliana na wanamgambo wa kiislamu wa Boko Haram katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa taifa hilo na kuyumbisha amani kabisa katika maeneo ya Niger Delta.