Yaya amchinja mtoto wa miaka 4 Moscow

Haki miliki ya picha AP
Image caption Yaya amchinja mtoto wa miaka 4 Moscow

Polisi huko Moscow wamemkamata mwanamke baada ya kupatikana amebeba kichwa cha mtoto.

Kanda ya video inamuonesha mwanamke huyo akitembea karibu na kituo cha basi akiwa amebeba kichwa hicho mikononi.

Alikamatwa na polisi na kupelekwa kufanyiwa uchunguzi wa akili.

Mwanamke huyo Gyulchekhra Bobokulova, kutoka jamhuri ya Uzbekistan anatuhumiwa kwa kumuua mtoto huyo msichana kabla ya kuchoma moto nyumba ya wazazi wake.

Picha za CCTV zinaonesha mwanamke huyo aliyevalia hijab akitembea nje ya kituo cha usafiri akiwa amebeba kichwa cha mtoto.

Afisa mmoja wa ulinzi anaonekana akimkabili na kumbwaga sakafuni kabla ya kumfunga pingu.

Bi Bobokulova amekamatwa na sasa anafanyiwa uchunguzi wa kiakili kubaini iwapo ana uwezo wa kubaini vitendo vyake.

Taarifa kutoka kwa afisi ya upelelezi wa jinai mjini Moscow inasema ’’ maafisa wameanzisha shughuli ya kubaini chanzo cha kifo cha mtoto ambaye kiwiliwili chake kilipatikana katika kitongoji cha Narodnoye Opolcheniye Magharibi mwa Moscow’’.

Haki miliki ya picha Ren TV
Image caption Picha za CCTV zinaonesha mwanamke huyo aliyevalia hijab akitembea nje ya kituo cha usafiri akiwa amebeba kichwa cha mtoto.

"'Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa yaya aliyekabidhiwa jukumu la kumtunza mtoto huyo mwenye umri kati ya miaka 3-4 alisubiri hadi wazazi wake na kakake mkubwa wakaondoka kabla ya kumuua na kisha kuchoma moto nyumba yao’’.

''Chanzo cha tukio hilo kwa hakika hakijabainika ila tumemkamata yaya huyo ambaye alizaliwa mwaka wa 1977 katika jamhuri ya Uzbekistan,'' taarifa hiyo iliongezea.

Afisa mwengine wa polisi ambaye hakutaka kutajwa anasema kuwa ''mtoto huyo alichinjwa na kiwiliwili chake kikachomwa moto.

Kichwa chake hakikupatikana kwenye eneo la tukio.''

Kwa mujibu wa jarida la kirusi la Life News, mwanamke huyo aliulizwa na askari polisi wa kituo cha usafiri cha Oktyabrskoye Polye, kitambulisho chake.

Hapo ndipo alipogutuka na kutoa kichwa cha mtoto huyo kutoka kwenye mkoba wake na kusema kwa sauti ya juu kuwa yeye ni gaidi na kuwa alikuwa malaika wa kifo na kuwa angejilipua.