Sanaa: Je, gaidi ni mtu wa aina gani?

Mwanabalozi
Image caption Mwanabalozi wa nchi ya Magharibi anatekwa na kuzuiliwa

Kila uchao, habari za magaidi kushambulia, kukamatwa au kuuawa hugonga vichwa vya habari. Mataifa ya Afrika Mashariki hayajaachwa nyuma na tatizo hili.

Lakini je, gaidi ni nani? Hili ni swali ambalo mchezo wa kuigiza kwa jina "A Man Like You" unatazamia kuutegua.

Mchezo huu, uliotungwa na Bi Silvia Cassini, unanuia kumaliza taharuki miongoni mwa jamii na hasa kulengwa kwa jamii ya Wasomali ambao wamelalamika Kulengwa na jamii nyingine kutokana na mashambulio ya wapiganaji wa Kiislamu wa al-Shabab lenye makao yake nchini Somalia.

Mchezo huu 'A Man Like You’ unasimulia maisha ya wanaume wawili, Abdi (Maina Olweny), raia wa Somalia ambaye anamteka nyara mwanadiplomasia wa taifa la magharibi (Tom Walsh) kwa siku 102.

Mhusika wa tatu Devina Leonard, mkewe Tom Walsh kwenye mchezo huu anawakilisha waathiriwa wa matukio ya kigaidi haswa familia zao, uchungu wanaopitia na pia ugumu unaowakumba wakati wanaomboleza ama kuendela na maisha bila jamaa wao.

Image caption Devina Leonard anayeigiza mkewe Tom

Maonyesho ya mchezo huo yataanza leo hadi tarehe 12 mwezi huu katika ukumbi wa Braeburn jijini Nairobi.

“Nia yangu haswa ni kuwafanya watu kufikiria kuhusu mada ambazo zitakuwa zikijadiliwa jukwaani kwa kina, ili kuleta mabadilika ya kimawazo kuhusu ugaidi, magaidi na pia dini. Vile vile tunataka kuwasilisha mchezo wa kuigiza wa kiwango cha juu”, Bi Cassini anaelezea.

Kenya imekumbwa na mashambulizi ya kigaidi kutoka kwa kundi la al-Shabab, ambayo yamesababisha vifo vya wengi, kuwaacha wengine bila jamaa wao, na kusababisha hali ya kutoaminiana kati ya Wakenya wengine na Wakenya wa asili ya Kisomali.