Mtangazaji afungwa kwa udhalilishaji

Haki miliki ya picha YouTube
Image caption Reham Saeed amefungwa kwa kosa la kumdhalilisha mgeni wa kipindi chake

Mtangazaji wa Televisheni nchini Misri amefungwa gerezani kwa kosa la kushindwa kulinda usiri wa mtu aliyemhoji kwenye kipindi chake.

Reham Saeed alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kwa kosa la kufanya mahojiano hayo, ambayo alieleza kuwa mwanamke aliyedhalilishwa kijinsia kuwa ilikuwa haki kwa yeye kutendewa hivyo.

Mgeni wake aliweka picha za video za mtu aliyemtendea vitendo vya kumdhalilisha kwenye mtandao wa Facebook baada ya Polisi kushindwa kumfungulia mashtaka.

Lakini Saeed, wakati wa mahojiano, alionyesha hewani picha za mwathiriwa huyo akiwa amevalia nguo fupi na zilizombana na kuonyesha maumbile yake.

Kisa cha kudhalilishwa kwa mwanamke huyo kilitokea kwenye duka moja kubwa mwezi Oktoba mwaka jana na kurekodiwa kwenye kamera.

Katika picha hizo alionekana mwanamke na mwanaume wakizozana, mwanaume alimkaribia mwanamke huyo na kumzaba kofi, kabla ya kukabiliwa na askari wa duka hilo, mwanamke alionekana akilalamika kwa polisi kuwa alidhalilishwa kijinsia.

Video hiyo baadae ilitazamwa na maelfu ya watu mitandaoni.

Mwanamke huyo alizungumza na Saeed katika kipindi chake na akamuuliza ''Unafikiri ulikuwa umevaa vizuri?'' kabla ya kumshutumu muathirika, siku ya tukio la kudhalilishwa mwanamke huyo, alikuwa amevaa suruali aina ya jeans na blauzi iliyokatwa mikono.

Mwanadada huyo alipeleka malalamiko kwenye vyombo vya sheria dhidi ya Televisheni na kipindi cha Saeed kiitwacho Sabaya al Khair ambacho baadae kilizuiwa kurushwa kwa muda.

Saeed alifanyiwa kampeni za chuki kwenye mitandao ya kijamii.

Siku ya Jumatatu alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na Mahakama ya mjini Giza na kutozwa faiani ya Pauni za Misri 10,000 (pauni za Uingereza 917). Ana haki ya kukata rufaa.