Yaya akiri kumuua mtoto Urusi

Image caption Yaya aliyekiri kumuua mtoto Urusi

Yaya mmoja nchini Urusi aliyetuhumiwa kwa kumuua mtoto wa kike na kumkata kichwa amesema kuwa ''Allah ndiye aliyemuagiza'' kutekeleza kitendo hicho.

Gulchekhra Bobokulova mwenye umri wa miaka 38 na mama ya watoto 3 alizungumza na maripota akielekea katika mahakama ya Moscow.

Bobokulova,ambaye ni Muislamu na raia wa Uzbekistan pia alijibu ''ndio'' alipoulizwa iwapo alitekeleza kitendo hicho.

Kamara za CCTV zilimuonyesha akiwa amevalia hijab ,akikaribia kituo kimoja cha treni akiwa na kichwa mkononi mwake.

Vyombo vya habari nchini Urusi vimeripoti kwamba alikitoa kichwa hicho katika begi lake na kuanza kupiga kelele kwamba angejilipua baada ya maafisa wa polisi kumtaka ajitambulishe.

Kanda nyengine ya video iliowekwa mtandaoni ilionyesha mwanamke aliyevalia nguo nyeusi akipiga kelele na kusema ''mimi ni gaidi,mimi ni kifo chenu''