Askofu Welby ahimiza maridhiano Burundi

Welby
Image caption Askofu Welby amesema suala la maridhiano linahitaji watu kujitolea

Askofu mkuu wa Canterbury Justin Welby amemaliza ziara yake nchini Burundi na kufanikiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa taifa hilo Pierre Nkurunziza.

Mzungumzo hayo yameangazia umuhimu wa kuwepo mazungumzo ya pamoja ili kuepusha mauaji yanayoendelea kufuatia vurugu zilizozuka kutokana na uamuazi wa Rais wa taifa hilo kuwania muhula mwingine wa Uongozi.

Mamia ya watu wameuawa kutokana na vurugu hizo huku maelfu wakilazimika kuikimbia nchi yao na kukimbilia nchi jirani.

Rais Pierre Nkurunziza katika mazungumzo hayo na kiongozi huyu wa kiroho, muda mwingi alionekana ni mwenye furaha na tabasamu mbele ya ambapo undani wa mazungumzo hayo ilikuwa ni kuhimiza ushiriki wa pande zote ili kuhakikisha kuwa amani ya kweli inafikiwa nchini humo.

Askofu Justin Welby amesema kuwa suala la maridhiano nchini Burundi linahitaji watu kujitoa mhanga.

Hata hivyo amesisitiza hatua za msingi za kuzingatiwa ili kuweza kufikiwa kwa amani ya kweli nchini Burundi.

Taifa la Burundi lililopata Uhuru wake 1962 na kupitia katika vipindi mbalimbali vya machafuko limejikuta katika upotevu wa hali ya amani katika kipindi kingine kufuatia uamuzi wa Rais wa taifa hilo Pierre Nkurunziza kuamua kuwania muhula mwingine hatua inayopingwa na upinzani nchini humo.