Ugiriki yazidiwa wimbi la Wahamiaji

Image caption Wahamiaji Ugiriki

Serikali ya Ugiriki imetakiwa kutangaza hali ya dharura kutokana na maelfu ya wahamiaji ambao wamekwama katika mpaka wa nchi hiyo na Macedonia.

Gavana wa kaskazini mwa Ugiriki, Apostolos Tzikostas ameielezea hali hiyo kuwa inahitaji huduma kubwa ya kibinadamu.

Ni idadi ndogo tu ya wanaotafuta makazi kutoka Syria na Iraq ndio wameruhusiwa kuvuka mpaka wa marcedonia tangu serikali ilipoweka kiwango cha mwisho kwa watu kuvuka.

Maelfu walikwama na kuweka kambi katika eneo la Idomeni,ambako wamekuwa wakipanga foleni ili kupata chakula.

Msemaji wa Kamishna wa maswala ya wakimbizi ndani ya Umoja wa Mataifa ,Babar Baloch ambaye yuko katika kambi hiyo amesema hali itakuwa mbaya zaidi kama hakuna hatua itakayochukuliwa.

Wakati huo huo shirika la madaktari wasio na mipaka (MSF) linajenga kambi ya wakimbizi kaskazini mwa Ufaransa ili kuwapatia makazi mapya watu ambao makazi yao nje ya Dunkirk yaliharibiwa vibaya na kimbunga mwezi uliopita.

MSF inasema kambi mpya itawahifadhi watu elfu moja mia tano. Shirika hilo la madaktari wasio na mipaka linashirikiana na uongozi wa maeneo hayo lakini Serikali ya Ufaransa inawataka watu kutafuta makazi katika makazi ya wakimbizi yaliyoidhinishwa.