Buhari: MTN iliisaidia Boko Haram kuua

Image caption MTN iliisaidia Boko Haram kuua watu 10,000.

MTN ilichangia mauaji ya wanigeria yaliyotekelezwa na wanamgambo wa Boko Haram.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amesema hayo katika mkutano na wanahabari akiwa na mgeni wake rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.

Zuma ameanza ziara ya siku mbili katika nchi yenye uwezo mkubwa zaidi kiuchumi (Nigeria) kwa nia ya kupunguza tofauti kati yao hususan kiuchumi.

Ziara hii inatarajiwa na wengi kuangazia tofauti katika uongozi wa rais wa Afrika Kusini ambaye amekumbwa na kashfa kadhaa za ufisadi na kiongozi wa Nigeria ambaye ametangaza vita dhidi ya ufisadi kuwa kipao mbele cha serikali yake.

Image caption ''Mnajua wazi kuwa nambari hizo ambazo hazijasajiliwa, zinatumika na magaidi na kuanzia mwaka wa 2009 hadi leo, Boko Haram, wameua zaidi ya wanigeria 10,000

Mawaziri kadhaa wameandamana na Zuma katika ziara hiyo ambayo inatarajiwa kuangazia pakubwa masuala ya uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Rais Buhari ameitaka mamlaka inayosimamia mawasiliano nchini humo kufanya majadiliano na kampuni hiyo ya mawasiliano ya Afrika kusini kuhusu mbinu za kulipa faini hiyo kwa malipo ya polepole.

Hii ndio mara ya kwanza kwa Buhari kulizungumzia hadharani swala la MTN ambayo ilipigwa faini ya dola bilioni 3.9 baada ya kukiuka makataa ya kuzima nambari zote za simu ambazo hazikuwa zimesajiliwa kwa mujibu wa sheria.

Buhari alisema kuwa haikuwa swala la kiuchumi.

''Ilikuwa ni swala la usalama wa taiafa '' alisema Buhari

''Mnajua wazi kuwa nambari hizo ambazo hazijasajiliwa, zinatumika na magaidi na kuanzia mwaka wa 2009 hadi leo, Boko Haram, wameua zaidi ya wanigeria 10,000 amini usiamini takribana watu 10,000.'' alisema Buhari.

Image caption Buhari: MTN ilisaidia Boko Haram kuua

''Mashirika mengine yalitekeleza matakwa hayo na MTN ikasitasita na hivyo ikachangia pakubwa kufanikisha mauaji ya watu'' alisema Buhari.

Aidha kampuni kadhaa za Afrika Kusini zimelalamika kuwa zimelengwa na vyombo vya dola nchini Nigeria pasi na sababu za kutosha.

Hata hivyo rais wa Nigeria Muhamadu Buhari amekariri kuwa sheria ni sharti itekelezwe kama njia moja ya kukabiliana na ufisadi nchini humo.