Zuma kujadili MTN na Buhari Nigeria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jacob Zuma

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ameanza ziara ya siku 2 nchini Nigeria ambapo ameratibiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Muhammadu Buhari mbali kabla ya kulihutubia bunge.

Ziara hii inatarajiwa na wengi kuangazia tofauti katika uongozi wa rais wa Afrika Kusini ambaye amekumbwa na kashfa kadhaa za ufisadi na kiongozi wa Nigeria ambaye ametangaza vita dhidi ya ufisadi kuwa kipao mbele cha serikali yake.

Mawaziri kadhaa wameandamana na Zuma katika ziara hiyo ambayo inatarajiwa kuangazia pakubwa masuala ya uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Aidha uamuzi wa serikali ya Nigeria wa kupiga faini kampuni ya simu za mkononi ya Afrika Kusini mabilioni ya madola, baada ya kuipata na hatia ya kutozima nambari za simu ambazo hazijasajiliwa, umejadiliwa.

Rais Buhari ameitaka mamlaka inayosimamia mawasiliano nchini humo kufanya majadiliano na kampuni hiyo ya mawasiliano ya Afrika kusini kuhusu mbinu za kulipa faini hiyo kwa malipo ya polepole.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Buhari ameitaka mamlaka inayosimamia mawasiliano nchini humo kufanya majadiliano na kampuni hiyo ya MTN

Kampuni hiyo ya MTN tayari imelipa dola milioni mia mbili hamsini ya faini hiyo na kwa sasa inaendeleza mazungumzo kuhusu jinsi ya kutatua suala hilo.

Aidha kampuni kadhaa za Afrika Kusini zimelalamika kuwa zimelengwa na vyombo vya dola nchini Nigeria pasi na sababu za kutosha.

Hata hivyo rais wa Nigeria Muhamadu Buhari amekariri kuwa sheria ni sharti itekelezwe kama njia moja ya kukabiliana na ufisadi nchini humo.