Kamanda wa IS anusurika shambulio la Marekani

Haki miliki ya picha AP
Image caption Tarkhan Batiravshili

Kundi moja la wachunguzi linasema kuwa kamanda mmoja wa ngazi za juu wa kundi la Islamic State alijeruhiwa vibaya lakini hakuuawa katika shambulio la angani lililotekelezwa hivi karibuni kaskazini mashariki mwa Syria.

Siku ya Jumanne,maafisa wa ulinzi wa Marekani walisema kuwa Tarkhan Batiravshili,raia wa Georgia anayejulikana kama Omar Shishani alifariki katika shambulio hilo karibu na Shaddadi siku ya Ijumaa.

Lakini kundi la wachunguzi hao nchini Syria lililo na makao yake makuu nchini Uingereza limesema kuwa lina habari kwamba alichukuliwa na kupelekwa kupata matibabu mjini Raqqa.

Hakuna tamko lolote kutoka kwa IS kuhusu ripoti hiyo ya kifo cha Shishani.

Mwaka uliopita ,Marekani ilitowa zawadi ya dola milioni 5 kwa yeyote yule ambaye angetoa habari za Shishani ambaye inasema ameshikilia nyadhfa kadhaa katika kundi hilo ikiwemo uwaziri wa vita.