Shambulio la Kigaidi laua Ivory Coast

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bassam, Ivory Coast

Watu 16 wameuawa nchini Ivory Coast katika shambulio llililofanywa kwenye hoteli ya kitalii ya Grand Bassam iliyoko ufukweni.

Rais wa nchi hiyo Alassane Ouattara, amesema wawili kati yao ni wanajeshi huku wavamizi sita pia wakiuawa karibu na mji wa Abidjan.

"Na bila shaka, kwanza kabisa, nitapenda kusema kuwa, hivi vitendo vya woga vya kigaidi kamwe hazitavumiliwa nchini Ivory Coast. Tumechukua hatua madhubuti dhidi yake''. amesema Ouattara.

Rais amesema hali ya usalama itazidi kudhibitiwa nchini kote.

Shambulizi hili limedhibitiwa ndani ya muda wa saa tatu mpaka nne,

Watu, waliokwenda katika eneo hilo, kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa juma, wamerudishwa mjini Abidjan.

Haki miliki ya picha no credit

Mashuhuda nao wanasema watu waliokuwa wamejifunika nyuso zao huku wakiwa na silaha walianza kurusha risasi katika fukwe, na baada ndio wakaingia hotelini.

Souleymane Kamagate ni miongoni mwa mashuhuda hao ambae alikuwa hotelini wakati wa tukio hilo na aliweza kupiga picha ya video ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii huku ikionyesha watu wanakimbia.

Wafuatiliaji wa mitandao ya wapiganaji wa kiislamu wanasema kundi la Al Qaeda lililopo kaskazini mwa Afrika limethibitisha kutekeleza shambulizi hilo.

Wakati huo huo, rais wa Ufaransa, Francois Hollande, ameliita tukio hilo kuwa ni ishara ya uwoga huku akiongeza kusema kuwa Ufaransa itatoa msaada wa kiiteligensia kwa Ivory Coast.

Ivory Coast imekuwa kisiwa cha amani magharibi mwa Afrika hadi pale tofauti za kisiasa zilipoibuka mwaka wa 2002 kati ya wenyeji wa Kaskazini na wale wa Kusini.

Tangu hapo nchi hiyo imekuwa ikishuhudia hali ya amani ambayo kila mara inatibuliwa na mapigano.