Muuaji wa Norway apiga saluti ya Nazi

Breivik Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Breivik alifungwa jela miaka 21 mwaka 2012

Mwanamume aliyefungwa jela kwa kuua watu wengi Norway amepiga saluti ya Nazi baada ya kufika kortini kujitetea akitaka apewe haki zaidi.

Anders Behring Breivik amesema kifungo chake ni kama “mateso” lakini serikali ya Norway imesema inafuata sheria.

Amepiga saluti punde tu baada ya kutolewa pingu.

Breivik aliuawa watu 77 mwaka 2011 alipolipua bomu katikati mwa Oslo na kisha kwenda kisiwa cha Utoya ambapo aliwaua kwa kuwapiga risasi watu waliokuwa kwenye kambi ya likizoni ya vijana.

Alifungwa jela miaka 21 mwaka 2012.

Breivik, 37, anasema si haki kwa serikali kufunga kifungo cha upweke akisema ameteswa sana kwa njia nyingi, ikiwemo kufungwa pingu muda mrefu.

Wakili wa Breivik Oystein Storrvik amesema hali ya mteja wake jela ni katili kushinda hukumu ya kifo ambayo ni marufuku Norway.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Breivik anasema maisha jela ni ya dhiki

Breivik anasema serikali ya Norway imevunja vifungu viwili vya Mkataba wa Ulaya kuhusu Haki za Kibinadamu. Kimoja ni kile kinachomhakikia mtu haki ya “maisha faragha na ya kifamilia” na “mawasiliano” na cha pili kinachoharamisha „ukatili dhidi ya binadamu”.

Awali, Bw Storrvik aliambia shirika la habari la AFP kwamba Breivik amefadhaika sana kutokana na upweke gereza la Skien.

Amesema amefadhaika kiasi kwamba ameshindwa kuendelea na masomo yake.

Septemba mwaka jana, Breivik alitishia kujinyima chakula hadi afe akilalamikia hali gerezani. Seli yake jela ya Skien ina televisheni na kompyuta lakini haina huduma za mtandao wa intaneti.

Kupitia barua kwa vyombo vya habari Norway na Sweden, alisema hutengwa muda mwingi na kwamba huruhusiwa kutoka nje ya seli saa moja kila siku.