Magufuli ataka wafanyakazi hewa wamalizwe

Magufuli Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Dkt Magufuli amesema wafanyakazi hewa hulipwa $1m kila mwezi

Rais wa Tanzania John Magufuli ametoa makataa ya siku 15 kwa wakuu wa idara na taasisi mbalimbali za serikali kufanya ukaguzi na kuwaondoa wafanyakazi hewa serikalini.

Rais Magufuli alitoa makataa hayo baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa 25 pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Valentino Mlowola na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata Jumanne, kwa mujibu wa taarifa ya ikulu.

Agizo hilo linahusu halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji, wizara na taasisi za Serikali.

Kwa mujibu wa gazeti la The Citizen, kuna takriban wafanyakazi hewa 2,500 katika utumishi wa umma nchini Tanzania.

Dkt Magufuli amenukuliwa na gazeti hilo akisema wafanyakazi hao hupokea mshahara wa takriban $1m (£700,000) kila mwezi.

Agizo hilo la kiongozi huyo ndiyo hatua yake karibuni zaidi katika kujaribu kukabiliana na ulaji rushwa serikalini na ufujaji wa pesa za umma.

“Nalitaka taifa hili lisonge mbele. Pesa tutakazookoa kwa kuondoa hawa wafanyakazi hewa zinafaa kusaidia katika ustawi,” amenukuliwa akisema.

Image caption Magufuli aliahidi kukabiliana na ulaji rushwa

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu, Dkt Magufuli pia amewataka Wakuu wa Mikoa wakasimamie utekelezaji wa elimu bure ya kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Hii ni pamoja na kuhakikisha shule zina madawati na majengo ya kutosha.