Manchester City watua robofainali UEFA

Kiev Haki miliki ya picha AP
Image caption Aguero akijaribu kuwapiga chenga wachezaji wa Dynamo Kiev

Manchester City wamefika robofainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza licha ya kutoka sare na Dynamo Kiev mechi ya marudiano.

City, waliokuwa mbele 3-1 kutokana na ushindi wa mechi ya kwanza, walidhibiti mechi ingawa waliwapoteza mabeki Vincent Kompany na Nicolas Otamendi kutokana na majeraha mapema.

Kipindi cha kwanza hakuna aliyetishia mwenzake lakini kipindi cha pili Jesus Navas aligonga mlingoti kwa kombora la chini naye Yaya Toure akatoa kombora ambalo lilitua mikononi mwa kipa.

Manuel Pellegrini, atakayeondoka mwisho wa msimu na nafasi yake kuchukuliwa na Pep Guardiola, anataka kumaliza kazi kwa kuwafanya City mabingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza.

Baada ya kushinda League Cup mwezi jana, matumaini halisi ya City kushinda kombe jingine msimu huu ni kutwaa ubingwa Ulaya.

Katika Ligi ya Premia, City wamo alama 12 nyuma ya viongozi Leicester.

Baada ya mechi meneja Pellegrini alithibitisha kwamba Kompany ameumia mguuni, mara yake ya 14 kuumia tangu ajiunge nao 2008.

Kompany alicheza mechi 19 kati ya 46 walizocheza City msimu huu na takwimu zinaonyesha huwa wanashindwa kutamba bila yeye.

Takwimu kutoka mashindano yote zinaonesha wamekuwa wakifungwa bao kila dakika 156 wakiwa naye kikosini lakini wanafungwa bao kila dakika 70 bila yeye.