Obama amwandikia barua mwanamke Cuba

Yarza Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ileana Yarza aliyemwandikia barua Rais Obama

Mwanamke mmoja aliyemwalika rais wa Marekani Barack Obama nyumbani kwake nchini Cuba amepokea barua ya majibu kutoka kwa rais huyo baada ya mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Marekani na Cuba kurejeshwa.

Ileana Yarza, mwenye umri wa miaka 76, aliandika kwa rais Obama mnamo mwezi Februari akimkaribisha kwa kikombe cha kahawa nyumbani kwake huko Havana.

Barua hiyo inayompatia asante Bi Yarza ilipelekwa nchini Cuba siku ya Jumatano.

Image caption Barua ya Obama

Zilikuwa barua za kwanza kuwasili nchini Cuba kutoka Marekani baada ya kipindi cha miaka 50.

Mawasiliano ya kutuma ujumbe wa moja kwa moja kati ya mataifa hayo mawili yalikatizwa wakati wa vita baridi,huku barua zilizoandikwa zikipitia mataifa mengine kama vile Mexico na Canada.

Bi Yarza aliandika kwa Obama mnamo tarehe 18 mwezi Februari baada ya kugundua kwamba anajiandaa kuizuru Cuba mnamo mwezi Machi, akimwambia: Raia wa Cuba ambao wangependelea kukutana nawe kibinafsi ni wachache.

Image caption Barua ilioandikwa na Obama

Rais Obama alimshukuru Bi Yarza kwa usaidizi wake akiongezea kuwa barua hiyo ni ishara ya uhusiano mzuri katika siku za usoni kati ya mataifa hayo mawili.

Na hakumpuuza kuhusu kikombe cha chai akisema kuwa atatafuta muda.