Kenya yathibitisha visa 2 vya homa ya manjano

Haki miliki ya picha SCIENCE PHOTO LIBRARY
Image caption Homa ya manjano

Kenya imethibitisha visa viwili vya ugonjwa wa homa ya manjano vilivyopatikana kwa mara ya kwanza baada ya kipindi cha miongo miwili.

Visa vyote viwili vilitoka nchini Angola ambapo mripuko wa ugonjwa huo umewauwa watu 150.

Kulingana na mwandishi wa BBC, Wakenya hao 2 waliwasili na ugonjwa huo kutoka Angola ambapo wamekuwa wakiishi na kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10.

Mgonjwa wa kwanza alifariki siku ya Jumatano katika hospitali ya Kenyatta huku mgonjwa wa pili akiendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo.

Maafisa wa afya wanasema wameimarisha doria yao huku wakiwahakikishia Wakenya kwamba hakuna hatari ya maambukizi ya moja kwa moja kupitia mbu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Chanjo ya homa ya manjano

Homa ya manjano ilikuwa imeangamizwa nchini Kenya.

Haina dawa,lakini ishara zake zinaweza kukabiliwa.

Angola inapambana na mripuko wa homa hiyo na imeanza kutoa chanjo kwa raia wake inayolenga watu milioni 7 katika eneo la Luanda lililoathirika.