Waingereza waliopiga picha ndege Kenya mashakani

Image caption Wapigaji picha wakichukua nambari za usajili za ndege

Raia wanne wa Uingereza waliokuwa wakipiga picha ndege nchini Kenya wameamrishwa kulipa faini ya pauni 1,400 ama wahudumie kifungo jela kwa kuchukua picha hizo katika uwanja wa ndege jijini Nairobi kinyume cha sheria.

Wanne hao kutoka Manchester nchini Uingereza walipatikana wakichukua picha hizo katika uwanja wa Wilson jijini Nairobi na wamekuwa wakizuiliwa kwa zaidi ya juma moja.

Wanaendelea kuzuiliwa na polisi hadi faini hiyo itakapolipwa.

Watu hao wanasema kuwa maafisa katika uwanja huo wa ndege waliwapatia ruhusa kufanya hivyo.

Lakini walizua tatizo la kiusalama walipopatikana katika baa ya uwanja huo wa ndege.

Baadaye walikiri mashtaka mawili ya kuingia na kupiga picha ndege bila ruhusa shtaka lililo na faini ya pauni 700 kila mmoja wao.