Kenyatta na Museveni kujadili bomba la mafuta

Kenyatta Haki miliki ya picha Uhuru Kenyatta Facebook
Image caption Rais Kenyatta na Rais Museveni watakutana ikulu ya Nairobi

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni watakutana leo jijini Nairobi kujadili ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kati ya nchi hizo mbili.

Mkutano huo utafanyika siku chache tu baada ya Uganda na Tanzania kuafikiana kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta kutoka bandari ya Tanga hadi nchini Uganda.

Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Kenya ni miongoni mwa miradi iliyo kwenye mpango mkubwa wa miradi ya miundo mbinu ya kanda ya kaskazini (NCIP).

Kampuni zinazozalisha mafuta nchini Uganda, kampuni ya Tullow kutoka Ireland, kampuni ya Ufaransa ya Total na kampuni ya CNOC kutoka Uchina, zimealikwa kuhudhuria mkutano huo baina ya Bw Kenyatta na Bw Museveni ikulu ya Nairobi.

Bomba hilo la mafuta lilikusudiwa kutumiwa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima hadi bandari ya Lamu, kupitia eneo lenye mafuta Kenya la Lokichar.

Viongozi hao wawili walikutana nchini Uganda Agosti mwaka jana na kuafikiana kwamba ujenzi wa bomba hilo ulifaa kuharakishwa.

Mpango huo unaonekana kushindana na mpango wa Uganda wa kushirikiana na Tanzania kujenga bomba la kusafirisha mafuta.

Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Rais Magufuli na Rais Museveni walipokutana mapema mwezi huu

Tanzania inataka ujenzi huo uanze haraka na wiki iliyopita Makamu wa Rais wa kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw Javier Rielo alimwambia Rais wa Tanzania John Magufuli, kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi huo haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.

Bomba hilo la kutoka Tanga hadi Uganda litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Utarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.