Magufuli: Atakayeshindwa umeya Dar akubali tu

matokeo Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Magufuli amezitaka pande zote ziwe tayari kukubali matokeo

Rais wa Tanzania John Magufuli ametoa wito kwa upande utakaoshindwa katika uchaguzi wa umeya Jiji la Dar es Salaam ukubali matokeo.

Uchaguzi huo utafanyika leo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kukataa ombi la Suzan Massawe na Saad Mohammed Kimji la kutaka uchaguzi huo usifanyike.

Hakimu Mkazi Mkuu Warialwande Lema alisema hakuona sababu za msingi kati ya zilizowasilishwa na walalamishi za kumfanya azuie uchaguzi huo.

Uchaguzi huo, ambao ulikuwa umeahirishwa mara tatu, utafanyika katika ukumbi wa Karimjee na ushindani utakuwa baina ya Isaya Mwita wa Chadema na Omary Yenga wa CCM.

Wajumbe 163 wanatarajiwa kushiriki, 87 wakiwa ni kutoka muungano wa upinzani wa Ukawa na 76 kutoka chama tawala cha CCM.

Kutakuwa pia na uchaguzi wa naibu meya.

Jumatatu, Rais Magufuli alizitaka pande zote kukamilisha mchakato wa kumpata meya badala ya kuendelea kulumbana.

Dkt Magufuli alisema upande wowote unafaa uwe tayari kupokea matokeo ya uchaguzi huo, ili meya apatikane na jiji liweze kuendelea na mipango yake ya kuwahudumia wananchi bila vikwazo.

"Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, na hiyo ndio demokrasia ya kweli" alisema Dkt Magufuli.